
MATEMBEZI YA WAKAZI WA DAR KUMBUKUMBU YA MIAKA KUMI TANGU KIFO CHA MBUNIFU MAARUFU WA MAJENGO BEDA AMULI KUPITIA MATEMBEZI YA KIHISTORIA YA URITHI WAKE
Familia, wasanifu majengo, wanafunzi na wananchi kwa ujumla wamealikwa kushiriki matembezi ya alfajiri yatakayopita katika alama mbalimbali za usanifu jijini Dar es Salaam tarehe 11 Julai 2026, kwa lengo la kumuenzi mtu aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kuunda taswira ya majengo ya jiji hilo.
DAR ES SALAAM — Asubuhi ya Jumamosi, tarehe 11 Julai 2026, mitaa ya Dar es Salaam itageuka kuwa ukumbusho hai wa maisha na mchango wa Mbunifu Majengo Beda Amuli. Tukio la Matembezi ya Kumbukumbu ya Miaka 10 ya Beda Amuli, lenye kaulimbiu ndogo “Kutembea Katika Urithi” (Walking Through a Legacy), litawakutanisha wasanifu majengo, wapangaji miji, wanafunzi, wanahistoria na wananchi kwa ujumla katika matembezi maalum yatakayounganisha majengo na maeneo muhimu yaliyoacha alama ya mchango wa mmoja wa wasanifu mashuhuri zaidi nchini Tanzania.
Tukio hilo limeandaliwa na familia ya marehemu kwa kushirikiana na Chama cha Wasanifu Majengo Tanzania (AAT), chini ya kaulimbiu “Kuilbuni Tanzania: Usanifu kwa Watu, Mahali na Kusudi” (Designing Tanzania: Architecture for People, Place, and Purpose).
Shughuli zitaanza katika Jengo la Old Boma, moja ya majengo ya kihistoria zaidi jijini Dar es Salaam, ambapo usajili na ugawaji wa fulana utaanza saa 12:00 alfajiri (6:00 AM), ikifuatiwa na hafla rasmi ya ufunguzi saa 12:30 alfajiri (6:30 AM). Matembezi yataanza rasmi saa 1:00 asubuhi (7:00 AM).
“Beda Amuli hakubuni majengo pekee. Alibuni maeneo ya kijamii na kiraia—mahali ambapo Watanzania wanaweza kufanya kazi, kujifunza, kufanya biashara na kukutana. Matembezi haya ni njia yetu ya kuhakikisha kwamba jiji alilosaidia kulijenga linaendelea kusimulia hadithi yake,” amesema Rais wa AAT, Mbunifu T’Chawi.
Njia ya Matembezi: Jiji Linasimulia Historia Yake
Washiriki wataanza safari yao kutoka Old Boma saa 1:00 asubuhi. Kituo cha kwanza kitakuwa eneo la Kilimanjaro/Hyatt saa 1:10 asubuhi, kikifuatiwa na Jengo la IFM saa 1:25 asubuhi, na baadaye Jengo la National Cooperative saa 1:40 asubuhi.
Matembezi hayo yatahitimishwa katika Soko la Kariakoo saa 2:05 asubuhi, eneo linalochukuliwa kuwa moyo wa biashara wa Dar es Salaam. Hapo kutakuwa na tafakari za pamoja, mahojiano na vyombo vya habari pamoja na hafla rasmi ya kufunga tukio hilo saa 2:30 asubuhi.
Washiriki wanashauriwa kuvaa fulana rasmi za “Walk of Legacy” pamoja na kofia maalum zinazopatikana kwa bei ya Shilingi 20,000 na Shilingi 10,000 mtawalia.
Waandaaji wamekaribisha michango na ushirikiano kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali ili kufanikisha tukio hilo.
Baada ya matembezi hayo, ibada maalum ya kumbukumbu itafanyika katika Kanisa la Anglikana la St Albans, jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi (10:00 AM).
Kuhusu Beda Amuli
Beda Amuli alikuwa mmoja wa wasanifu majengo wa kwanza na wenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania. Kazi zake zimeacha alama ya kudumu katika mandhari ya Dar es Salaam kupitia usanifu wa majengo ya umma, biashara, elimu na taasisi mbalimbali.
Falsafa yake ya usanifu iliona majengo kama nyenzo ya kujenga utambulisho wa taifa na kutoa huduma kwa jamii. Alifariki dunia miaka kumi iliyopita, na matembezi haya ya kumbukumbu ni juhudi za jamii kuhakikisha kuwa urithi wake wa kitaaluma hauishii kukumbukwa pekee, bali unaendelea kuhamasisha kizazi kipya cha Watanzania.
MAELEZO YA TUKIO
Tarehe: Jumamosi, 11 Julai 2026
Mahali pa Kukusanyika: Old Boma, Dar es Salaam — kuanzia saa 12:00 alfajiri
Matembezi Yaanza: Saa 1:00 asubuhi
Ibada ya Kumbukumbu: Kanisa la St Albans Anglican, saa 4:00 asubuhi
Bei ya Fulana: Shilingi 20,000
Bei ya Kofia: Shilingi 10,000
KWA MAWASILIANO:
Elizabeth Amuli
Mratibu wa Matembezi, Kamati ya Kumbukumbu ya Beda Amuli
Simu: 0747 222 392
#BedaAmuliWalk
Translated by Msimulizi
Discover more from Msimulizi Community News
Subscribe to get the latest posts sent to your email.
